Skip to main content

Shirika la Haki Afrika laishinikiza serikali ya Kenya na Tanzania kutafuta suluhu la haraka kufuatia kuzuiliwa kwa Hamisi Zuma.

Afisa wa kitengo cha dharura kutoka shirika la Haki Afrika Mathias Shipeta Picha (Maktaba)
Na Mwarandu Kombe

Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika limeitaka serikali ya Kenya na Tanzania kuingilia kati ili kutafuta suluhu la haraka kufuatia kuzuiliwa kwa mkenya Hamisi Zuma Madilo nchini Tanzania.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari afisa wa kitengo cha dharura wa shirika hilo Mathius Shipeta amesema shirika hilo limeghadhabishwa na hatua ya serikali ya Tanzania kumzuilia mkenya huyo asiyekuwa na hatia.

Ameongeza kuwa licha ya mataifa ya Kenya na Tanzania kutia saini mkataba wa wa makubaliano  baina ya nchi hizi mbili maeneo ya mpakani  bado mkataba huo unakiukwa.

Ametaja hatua ya kumzuilia mkenya huyo kama ukiukaji mkuu wa haki za binadamu.

Kulingana na taarifa ya hivi punde kutoka kwa afisa huyo maafisa wa shirika hilo wakiandamana na familia ya mhusika wako eneo la Horo Horo nchini Tanzania.

Mkenya huyo alikamatwa na maafisa wa mpakani nchini Tanzania usiku wa kuamkia siku kuu ya krismasi huku akiendelea kuzuiliwa hadi sasa.

Amezitaka idara husika nchini Tanzania kuheshimu sheria na haki za kibinadamu na kumuachilia huru mkenya huyo.


Comments